Waziri Mkuu: Vijana Jitokezeni Mlime Korosho
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu lina fursa nyingi.
“Mahitaji ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika mahotelini na kwenye mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa,” alisema.
Ametoa wito huo Jumapili, Desemba 31, 2017 wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni:“Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.
Waziri Mkuu alisema anaamini kuwa kijana yoyote mwenye nguvu ya kufanya kazi hawezi kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa. “Kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche 37 hadi 40. Kuna mtu atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” aliuliza.
Waziri Mkuu alisema kilimo cha korosho ni rahisi lakini pia kilimo cha korosho ni rafiki wa mazingira, kwani miti ikikua inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua. Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya Lindi, Mtwara, Ruvuma Pwani na Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika kuwa zao hilo linaweza kustawi bila shida.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.
“Leo tumeanza usambazaji wa miche ya bure hapa Ruangwa ambao najua utafuatiwa na wilaya nyingine hapa nchini. Nimeelezwa kwamba mche wenye kutoa mazao mengi ni wa kuanzia miaka mitatu hadi saba, kwa umri huu miche ya korosho inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama ambavyo mtashauriwa na maafisa kilimo ili wakati wa palizi ya hayo mazao, shamba lako la korosho libakie kuwa safi,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.
Mapema, akitoa taarifa ya taarifa ya uzalishaji wa miche ya mikorosho msimu wa 2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. Ramadhani Kaswa alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo uliweka lengo la kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.
“Hadi mwisho wa msimu huu, jumla miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima sawa na asilimia 71.6 ya lengo lililowekwa. Kati ya hiyo, Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri ya Lindi miche 100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale miche 106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya Ruangwa miche 177,862,” alisema.
“Miche hii iligawanywa kwa wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao. Zoezi la tathmini ya miche iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye halmashauri zote za mkoa,” aliongeza.
Bw. Kaswa alisema kutofikiwa kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa, na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.
Alisema kwa msimu huu wa 2017/2018, mkoa uliweka lengo la kuzalisha miche ya mikorosho iliyobebeshwa na isiyobebeshwa 7,132,000. Kati ya hiyo, Wilaya ya Kilwa walilenga miche 1,122,000, Lindi Vijijini 1,550,000, manispaa ya Lindi 1,000,000, Liwale miche 450,000, Nachingwea miche 1,810,000 na Ruangwa miche 1,200,000.
“Hadi kufikia tarehe 29 Desemba, 2017 tayari miche 4,974,425 ilikuwa imezalishwa na iko tayari kwa kupandwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa kama ifuatavyo:- Kilwa miche 772,000, Lindi Vijijini 1,160,455, manispaa ya Lindi 771,440, Liwale miche 266,000, Nachingwea 991,070 na halmashuri ya Ruangwa imezalisha miche 1,013,460,” alisema.
Sherehe hizo za uzinduzi wa upandaji miche mipya zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,