Tundu Lissu Kataja Kitu Ambacho Hatakisahau Tangu Apelekwe Nairobi
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu amekiri kwamba hatakuja kusahau tukio la mkazi wa Iringa aliyekwenda hospitali Nairobui alikolazwa kwa ajili ya kumuombea ili apate kupona baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Lissu ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini, amedai kwamba mama huyo alimgusa sana kwa upendo aliouonyesha juu yake huku akizingatia kwamba ametokea mbali sana huku akionekana ni mtu wa hali ya chini.
"Ukiwa mgonjwa kisha akaja mtu kukutembelea ni faraja sana. Nawashukuru maelfu ya watanzania na watu wote waliofika Nairobi kunijulia hali. Lakini sitakaa kuweza kumsahau mama mmoja aliyetoka Iringa kwa ajili ya kuja kuniombea," Lissu.
Lissu ameongeza "Aliniambia Mheshimiwa nimetokea Iringa na mpaka nimefika hapa nimetumia siku tano. Nikamwambia mama asante niombee kisha akapiga magoti na kuniombea. Alinigusa sana na ukimuangalia mama yule unatambua kabisa hajatokea mjini na hata hali yake ya uchumi siyo nzuri lakini ulikuwa ni upendo wa ajabu ambao ulinigusa sana".
Mbunge Lissu yupo hospital ya Nairobi akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulika huko mkoani Dodoma wakati akiwa ametokea kazini (bungeni) Septemba 07, 2017