TRA Wakomaa na Askofu Kakobe.....Wadai Hawana muda wa Kubishana nae Zaidi ya Kuchunguza Utajiri wake
TRA Wakomaa na Askofu Kakobe.....Wadai Hawana muda wa Kubishana nae Zaidi ya Kuchunguza Utajiri wake
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imemuibukia kivingine, Askofu wa Kanisa la Full Gosper Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, kuhusu utajiri alionao ikisema haina muda wa kulumbana naye, bali inatekeleza maelekezo ya Kamishna Mkuu.
Aidha, mamlaka hiyo imesema haitaki kuwa kwenye malumbano na askofu huyo wakati ikiendelea na uchunguzi dhidi ya vitega uchumi vyake na kuangalia kama analipa kodi ya serikali.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, jana alisema maofisa wao wanaendelea kutekeleza tamko la Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, la kuchunguza utajiri wa Askofu Kakobe.
"Sisi (TRA) hatutaki kuwa kwenye malumbano na Kakoke, tulichosema tumeishia hapo. Alichosema Kamishna Mkuu tunaishia hapohapo, hatutakiwi kujibishana naye," Kayombo alisema.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumamosi, Kichere alisema mamlaka yake imeipokea kwa furaha kauli ya Askofu Kakobe kuhusu utajiri wake na inataka kujiridhisha vyanzo vya utajiri huo.
Kichere alisema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi, lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka pekee.
Alisema wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za TRA.
Kauli iliyoleta utata na kuibua uchunguzi huo ni ya Askofu Kakobe kukaririwa wiki iliyopita akidai ana fedha nyingi kuliko serikali na anao uwezo wa kumkopesha waziri pindi akiombwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, juzi ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza kufanya uchunguzi dhidi yake, Askofu Kakobe alieleza historia ya maisha yake, mali za kanisa na zake na misukosuko aliyopitia na kusisitiza kuwa tafsiri iliyofanyika dhidi ya kauli yake kuhusu utajiri ni ya kimwili na siyo ya kiroho. Alidai kauli yake ilimaanisha yeye ni tajiri wa kiroho na si fedha.
Askofu Kakobe aliishauri TRA kutohangaika naye, badala yake ikatafute fedha mahali kwingine akieleza kuwa ana nyumba moja iliyopo Kijitonyama jijini na aliijenga mwaka 1986 kwa gharama ya Sh. milioni mbili ikiwa ni pamoja na gharama za kiwanja.
Huku akishangiliwa na waumini wa kanisa lake kwenye ibada ya kuuaga mwaka 2017, Askofu Kakobe pia alidai kuwa mwaka 1995 alinunua gari aina ya Nissan Patrol kwa kutumia sadaka za washirika wa kanisa na hivi karibuni waliibuka watu waliochangishana na kumnunulia gari jingine.
Alidai kuwa hata kwao Kakonko, Kigoma hajawahi kujenga hata choo na kilichopo ni makaburi ya wazazi wake waliozikwa kwenye eneo la kuingia kwenye nyumba iliyojengwa na wazazi wao.
Askofu Kakobe pia alidai kuwa kanisa la FGBF ndani na nje ya nchi halina mradi wowote wa kiuchumi kama shamba au hoteli na akasisitiza serikali ichunguze kote huko.
Alibainisha kuwa makusanyo yote ya sadaka huhifadhiwa kwenye akaunti iliyofunguliwa mwaka 1990 katika Benki ya NBC na ni mali ya bodi ya wadhamini ambayo imesajiliwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).