Spika Ndugai Amjibu Tundu Lissu
Spika wa Bunge Job Ndugai amefunguka na kusema Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na familia yake hawatambui kuwa Serikali hasa Bunge limeanza kufanya mazungumzo na watu wanaotaka kumsafirisha kwenda nje kwa matibabu zaidi.
Ndugai amedai anatambua kuwa Tundu Lissu atasafirishwa na kwenda kwa matibabu zaidi nje ya Kenya ingawa hajajua ni lini lakini amesema kuwa watu ambao wamepanga kumpeleka huko kwenye matibabu tayari walishamtafuta yeye na kusema watashirikiana nao katika masuala ya matibabu.
"Ni kweli kwamba atapelekwa nje zaidi ya Nairobi ila bado sijui mpaka sasa ni lini kwa kuwa sijajua tarehe bado japo nadhani itakuwa hivi karibuni na wale wanaomgharamia kumpeleka nje wameshawasiliana na mimi na hakika familia ya Lissu hata Tundu Lissu mwenyewe hajui hilo, anafikiri ni wao peke yao lakini najua na walishafika kwangu na kusema watagharamia wao" alisema Ndugai
Spika Ndugai alizidi kueleza kuwa endapo watakubaliana na watu hao basi wao kama Serikali watagharamia katika mambo mengine ambayo yatawashinda hao wadau ambao walimfuata na kuongea naye.
"Gharama ambazo sisi tunaweza kuziingia endapo tutakubaliana na maamuzi hayo kufanyika itakuwa katika yale mambo mengine yanayobakia ambao wale kama wadau, wawezeshaji, wanaotusaidia hawataweza kutoa na ili liafikiwe lazima tuwe na uhakika kitu gani kinalipiwa na kitu gani hakilipiwi vinginevyo tutalipa mara mbili mbili sisi tunalipa wenzetu wanalipa ambapo kidogo italeta mchanganyiko usiokua na afya" alisisitiza Ndugai
Mwaka jana Tundu Lissu alidai kuwa Serikali pamoja na Bunge bado walikuwa hajachangia jambo lolote katika matibabu yake ambayo yanaendelea mpaka sasa nchini Kenya jijini Nairobi kufuatia shambulio lake la kupigwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma.