Onyo Zito Latolewa Kampeni za Uchaguzi Katika Jimbo la Nyalandu
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, ameonya kuwa watu watakaovuruga mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Singida Kaskazini, serikali itawashughulikia kwa mujibu wa sheria.
Dk. Nchimbi alitoa onyo hilo katika Kijiji cha Mtinko Wilaya ya Singida Vijijini alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya tano kwenye uzinduzi wa kampeni hizo.
Alisisitiza kwamba ili watambue kuwa ni mtumishi aliyetumwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ajitokeze mtu yeyote na kuthubutu kuvuruga ratiba ya mikutano ya kampeni.
Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa mikutano ya kampeni itakuwa salama pamoja na uchaguzi huo kwani serikali imejipanga kikamilifu kudhibiti yeyote atakayeonekana anataka kuvuruga uchaguzi huo.
“Na ole wake na atokee mtu yeyote yule mwingine atakaeingilia katika njia hii ya uchaguzi salama, amani na utulivu ndipo mtakapotambua kwamba nimetumwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema na kuongeza:
“Jiandaeni vizuri na wakati wa kura mjitokeze kwa wingi kupiga kura na kumchagua mgombea wa CCM, na siyo mwingine.”
Dk.Nchimbi aliyataja baadhi ya mafanikio yaliyopo katika jimbo hilo ni bomba na mafuta kutoka Horiri Uganda hadi Tanga ambalo kwa Singida Kaskazini lina sifa ya pekee yake na litakuwa limenyanyuka kiuchumi kuliko sehemu yeyote litakapopita.
“Na hapa Singida Kaskazini kutajengwa kambi, patajengwa kituo watakuja wataalamu na mabingwa wa hilo bomba ambao watakaa hapa kwa zaidi ya miaka mia moja, hawatakaa pengine bali watakuja kukaa Singida Kaskazini,”alisema.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu (CCM), kujiuzulu na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).