Mjerumani auawa kwa kisu Zanzibar....Wanawake Wanne Watiwa Mbaroni
Raia wa Ujerumani Gerd Winkdl (60), amefariki dunia Zanzibar akidaiwa kuchomwa kisu na marafiki zake wa kike kutokana na wivu wa kimapenzi huku wanawake wanne wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na kifo hicho.
Tukio hilo lilitokea usiku wa mkesha wa Mwaka Mpya Shangani Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Hassan Nassir Ali, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:30 usiku baada ya kusherehekea Mwaka Mpya wa 2018 akiwa na marafiki zake hao.
Alisema kabla ya kukutwa na umauti, Winkdl akiwa na marafiki zake wanne ambao wanadaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi, waligombana na baadaye ugomvi huo kusababisha kuchomwa kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Ali alisema watuhumiwa hao wanne ambao wote ni wanawake, raia wa Tanzania na Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikiliwa kwa ajili ya kuwahoji na kukamilisha taratibu za kiuchunguzi.
"Inasemekana wote walikuwa wameshalewa na inadaiwa kuwa chanzo cha ugomvi ni wivu wa kimapenzi, lakini tunaendelea na uchunguzi," Kamanda huyo alisema.
Aidha, Kamanda Ali alibainisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mnazimmoja kisiwani hapa.
Aliongeza kuwa raia huyo wa kigeni alikuwa anaishi Zanzibar akiwa ni msimamizi wa mapishi katika hoteli moja ya kitalii kisiwani hapa.