Mawaziri, wakuu wa Wilaya wa awamu zilizopita kidedea ndani ya Uchaguzi CCM
Wanachama waliokuwa mawaziri na wakuu wa wilaya katika uongozi wa Serikali za awamu zilizopita, wameibuka kidedea kwenye uchaguzi ndani ya CCM unaoendelea kote nchini.
Mawaziri wawili wa zamani, Kate Kamba na Anthony Diallo wameibuka kuwa wenyeviti wa mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.
Kamba aliwahi kuwa naibu waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto na naibu waziri wa Viwanda na Biashara kati ya mwaka 1994 na 1995. Pia, aliwahi kuwa mbunge wa Afrika Mashariki.
Kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2000 na 2008, Diallo aliwahi kuwa naibu waziri wa Maji na Mifugo, naibu waziri wa Viwanda na Biashara; waziri wa Maendeleo ya Mifugo na waziri wa Maliasili na Utalii.
Juzi, msimamizi wa uchaguzi wa CCM mkoani Dar es Salaam, William Lukuvi alimtangaza Kamba kuwa mshindi baada ya kupata kura 443. Wapinzani wake, Brigedia Jenerali mstaafu Ryakitimbo Magige alipata kura 22 na Malima Bunara kura 12.
Kamba alisema chama hicho kina mizizi katika jumuiya zake na kwamba kuna wakulima na wafanyakazi ambao hawana chama, hivyo viongozi washirikiane ili kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Diallo, aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, aliibuka mshindi kwa kupata kura 555 kati ya 1,086 zilizopigwa akiwabwaga wapinzani wake watatu, akiwamo aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki aliyepata kura 520.
Wagombea wengine waliowania kiti hicho ni Enock Masele aliyepata kura tano na Richard Lukambula aliyepata kura sita.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi juzi, Diallo alisema: “Niwapongeze wote mlionipa ushindi huu hata wale ambao kura zao hawakunipaa nawashukuru pia. Zaidi natamani tuwe wamoja ili kuendelea kukipa ushindi chama chetu kizidi kushika dola.”
Sadiki alisisitiza kuendeleza mshikamano na kumuunga mkono aliyeshinda, huku Lukambula akiwaomba msamaha wajumbe kwamba huenda aliwakosea wakati wa kampeni ndiyo maana wakaamua kumpa kura chache. Hata hivyo aliahidi kumpa ushirikiano kiongozi aliyechaguliwa.
Juzi, Diallo alieleza kukerwa na kitendo cha maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kusimamisha gari lake na kulipekua alipokuwa kwenye kampeni wilayani Ukerewe.
Akizungumza wakati wa kuomba kura, alisema amesikitishwa na kutofurahishwa na kitendo cha maofisa hao.
Mkoani Singida, waliokuwa wakuu wa wilaya katika Serikali ya Awamu ya Nne walishinda nafasi za uongozi katika Jumuiya ya Wazazi ya CCM.
Wakuu hao wa zamani ni Erasto Sima, ambaye alishinda nafasi ya mwenyekiti wa mkoa wa jumuiya hiyo, wakati Francis Mtinga alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu CCM na Baraza Kuu Wazazi. Mtinga aliwahi kuwa mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Mkoani Rukwa, Rainer Lukara alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM wa mkoa akimbwaga Hipolitus Matete aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyesimamia uchaguzi huo alimtangaza Lukara aliyepata kura 357 kuwa mshindi katika nafasi ya mwenyekiti akimbwaga Matete aliyepata kura 148, huku aliyekuwa mkuu wa wilaya, Kanali John Mzurikwao akipata kura tisa na Victor Chang’a kura moja.
Lukara aliwataka wagombea kuvunja kambi, akisema katika uongozi wake atahakikisha jumuiya za CCM zinakuwa imara.
Alisema atahakikisha rasilimali zilizopo ndani ya CCM zinawanufaisha wanachama wote, wakiwamo mabalozi wa nyumba 10 ambao wamekuwa wakifanya kazi za kukijenga chama hicho kuanzia ngazi ya matawi na shina.
Mkoani Tanga, Henry Shekifu alitetea nafasi ya uenyekiti wa mkoa aliyoshikilia kwa miaka mitano. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Martine Shigella juzi, ulimalizika saa 9:00 usiku baada ya wajumbe kurudia kupiga kura kwa nafasi ya mwenyekiti.
Shekifu alishinda kwa kupata kura 609 kati ya 1,163 zilizopigwa, akimshinda Balozi Abdi Mshangama aliyepata kura 530 .
Katika awamu ya kwanza, Balozi Mshangama alipata kura 528 ambazo hazikuvuka nusu ya kura zote.
Mgombea mwingine aliyewania nafasi hiyo ni mbunge wa zamani wa Pangani, Rished Abdallah aliyepata kura 133 hivyo kulazimika kuwaachia Mshangama na Shekifu kuchuana katika duru la pili.
Katika mkutano huo, aliyekuwa mgombea ubunge wa Bumbuli katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia Chadema, David Chanyeghea alitangaza kuhamia CCM.
Imeandikwa na Pamela Chilongola, Ngollo John, Johari Shani, Mussa Mwangoka, Gasper Andrew na Burhani Yakub
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps