CUF ya Maalim Seif Yachekelea Maulid Mtulia kujiuzulu Ubunge
Uamuzi wa Maulid Mtulia kujivua ubunge na uanachama haujakishtua chama chake cha CUF, badala yake kimesema bado wengine wawili ambao kingependa waondoke haraka.
Hilo lilisemwa jana na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaongoza upande mmojapo kati ya mbili zinazokinzana. Upande mwingine unaongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
Naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa, Mtulia ni mmoja wa wabunge watatu wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.
“Hatukutarajia kama Mtulia ataondoka wakati huu, bali tulijua ataendelea kudumu. Lakini kama ameondoka ni faraja kwetu kwa sababu katika mipango yetu tulishamuondoa,” alisema Mazrui.
“Tunawaombea dua wale wawili waliobaki waondoke hata leo kwa sababu kuendelea kukaa kwao ndani ya CUF ni kukidhoofisha chama hiki.”
Mazrui aliwataka wabunge kutoshangaa endapo wenzao hao watatangaza kujiuzulu nafasi zao akidai kuna mipango inaendelea kupangwa ili kufanikisha mchakato huo.
“Narudia tena na waondoke, tena waondoke haraka. Ninawahakikishia wana CUF kuwa chama hiki kipo imara na wasiwe na hofu,” alisema Mazrui.
Alisema CUF ni taasisi imara na kati ya wabunge 40, watatu alidai wamekuwa wakikivuruga chama hicho kwa kushirikiana na Profesa Lipumba.
Akizungumzia kuondoka kwa Mtulia, alisema wakati mwingine akifa mgonjwa uliyemuuguza muda mrefu unamshukuru Mungu.
“Tunamshukuru Mungu maana tumeuguza vya kutosha. Haikuwa bahati yetu,” alisema.