CUF ya Lipumba Yawaomba radhi wapiga kura Kinondoni Baada ya Mbunge wake Maulid Mtulia Kujiuzulu
Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Profesa Ibrahim Lipumba kimewaomba radhi wapiga kura wa jimbo la Kinondoni baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia chama hicho, Maulid Mtulia kujiuzulu.
Kauli imetolewa leo, Jumatatu Desemba 4, 2017 na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya wakati akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya chama hicho Buguruni.
Amesema CUF iliwaaminisha wakazi wa Kinondoni kwa kumpeleka Mtulia kugombea jimbo hilo kwa kuwa ni mtu makini na mambo mengi alishaanza kuyatekeleza ikiwamo kuzuia bomoa bomoa lakini wanasikitika kujiuzulu kwake.
"CUF haikutarajia kuingia katika uchaguzi mdogo hasa jimbo la Kinondoni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 labda kingetokea kifo. Tunawaomba radhi wakazi wa Kinondoni," amesema Kambaya.
Kambaya amesema sababu za kujiuzulu alizozitoa Mtulia ni za msingi kwake lakini kwao hazina maana wala mashiko.
Desemba 2, Mtulia alitangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishia na mtu yoyote na ameamua kuhamia CCM.