Tambwe arejesha furaha Yanga
MSHAMBULIAJI AMISSI TAMBWE.
Tambwe amekosa mechi zote za Ligi Kuu Yanga tangu kuanza kwa msimu huu, lakini sasa inaelezwa kuwa anaweza kushuka dimbani baada ya mchezo ujao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mechi ijayo ya Yanga itakuwa dhidi ya Tanzania Prisons itakayopigwa Uwanja wa Uhuru Jumamosi ya Novemba 25, mwaka huu.
Katika mazoezi ya jana asubuhi, Tambwe alifanya mazoezi mepesi ya peke yake na ametakiwa kufanya hivyo kwa angalau siku tatu kabla ya kuanza kujifua kamili na wenzake.
Meneja wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Hafidh Saleh, aliliambia Nipashe baada ya mazoezi hayo jana kwamba, pamoja na Tambwe kuanza kujifua, hatocheza mchezo wa Jumamosi.
“Kwa mchezo wa Jumamosi hatoweza kucheza kwa sababu daktari amemtaka kuanza na mazoezi mepesi kwa siku tatu baada ya hapo ataungana na wenzake kwa program za mwalimu (George Lwandamina),” alisema Saleh.
Usajili sasa siri
Katika hatua nyingine, benchi la ufundi la timu hiyo, bado halijaweka wazi kama litahitaji kufanya usajili katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa leo.
“Kwa kweli suala la usajili bado, kocha amerejea jana na ni mpaka atakapokutana na uongozi ndipo tutajua kama kuna usajili utafanyika,” alisema Saleh.
Alisema kocha Lwandamina alirejea nchini jana alfajiri akitokea kwao Zambia na leo ataungana na kikosi chake kuendelea na program ya mazoezi kujiandaa na mchezo wa Jumamosi huku wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wakipewa mapumziko ya siku moja.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps