Skip to main content

Waziri Mkuu akoleza moto sakata la vyuo vikuu 19 kufungiwa

Waziri Mkuu akoleza moto sakata la vyuo vikuu 19 kufungiwa


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepigilia msumari sakata la vyuo vikuu 19 kuzuiwa udahili na kuvitaka kufanyia kazi kasoro zilizoainishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) badala ya kulumbana.

Juzi, TCU ilivifungia vyuo 19 kudahili wanafunzi pamoja na kuzuia kozi 75 katika vyuo 22 nchini kutokana na kasoro mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya siku tatu ya Vyuo Vikuu nchini, Majaliwa alivitaka vifuate utaratibu na si vinginevyo.

Waziri Mkuu pia alitoa wito kwa TCU na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), kuhakikisha kuwa programu zote zinazotolewa na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kupata ajira au kujiajiri na kuhimili ushindani kimataifa.

Aliwataka waweke mikakati ya kuinua viwango vya taaluma ili kuwa na tija kwa maendeleo ya nchi na dunia kwa ujumla, huku akizitaka taasisi za elimu ya juu kuangalia tena mitalaa yake ili iende sambamba na dunia ya kazi na ajenda za maendeleo ya Taifa.

“Waimarishe mfumo wa ithibati na ubora wa elimu na mafunzo ili kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu shahada wanachangia maendeleo,” alisema Majaliwa.

Mbali ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila pia alivitaka vyuo vikuu vilivyoandikiwa barua na kupewa maelekezo ili kufanya marekebisho, kuyawasilisha TCU badala ya kutafuta njia ya mkato.

Aliwataka wenye vyuo kutatua changamoto zao na kuwaambia wasitarajie kwamba watatumia ofisi yoyote ya Serikali au kiongozi kuwasaidia.

Alisema wizara haitakivumilia chuo kikuu chochote kitakachotoa elimu yenye upungufu.

Profesa Msanjila alisema TCU itawachukulia hatua wanaoendelea kujitangaza licha ya kufungiwa kudahili, kwa sababu kufanya hivyo ni kuwadanganya wananchi.

Pia, alivitaka vyuo vikuu kufuata ada ya usajili iliyoelekezwa na Serikali ambayo haipaswi kuzidi Sh10,000.

Maoni ya wadau

Msimamo huo wa Serikali umeungwa mkono na baadhi ya wadau. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Profesa Joe Lugalla alisema hatua hiyo ni sahihi na inastahili kufanyiwa kazi.

Alisema waliliona hilo mapema ndiyo maana wapo makini katika udahili na kozi wanazotoa, ubora wa kozi hizo, na kuwa na walimu waliobobea katika taaluma mbalimbali.

Alisema wamejikita katika mambo mawili, afya na elimu, kwa sababu hakuna nchi itakayoendelea kama wananchi hawana afya na utaalamu wa kuelewa matatizo na kutafuta mbinu za kuyatatua.

Msemaji wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mwenge cha Moshi, Athanas Sing’ambi alisema chuo hicho kimefungiwa kudahili kozi moja ya ‘Bachelor of Arts in Philosophy with Ethics’.

“Tumekubali kwa sababu kozi hiyo haikuwahi kuwa na wanafunzi,” alisema.

Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John ambaye hakuwa tayari jina lake kutajwa gazetini alilalamikia uhakiki huo kwa ujumla.

Alisema walipewa barua wiki mbili zilizopita na wamejibu baada ya wiki moja, lakini wanashangaa kabla hawajapata majibu, jina la chuo chao limo katika orodha ya waliozuiliwa kudahili.

“Sipingi maboresho, bali kama wanataka sekta binafsi iwe imara, tungekaa pamoja wakatupa maelezo tukashirikiana nao kutatua changamoto zilizojitokeza kuliko kutukomoa hasa katika kipindi hiki cha udahili,” alisema.

TCU wamezitaja sababu za kuvifungia vyuo hivyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na walimu, vifaa na kutokidhi vigezo kitaaluma.

Popular posts from this blog

Jinsi ya kutengeneza SABUNI ya kipande YA KUGANDISHA

Jinsi ya kutengeneza SABUNI ya kipande YA KUGANDISHA Utengenezaji wa sabuni hii una njia nyingi Hatua  ya kwanza Chemsha vipimo 7 vya mafuta ya mawese au mafuta ya shea hadi ifikie hatua ya kimiminika chuja na yaweke kwenye chungu cha mfinyanzi au chombo cha plastiki. Hatua ya pili Pima vipimo 5 vya maji baridi kwenye chombo cha plastiki ongeza kipimo 1cha sodium hydroxide kwa uangalifu mkubwa kwenye maji acha hadi mchanganyiko huo uyeyuke. Subiri mchanganyiko wa sodium hydroxide na mafuta ukaribie kupoa. Hatua ya tatu Taratibu ongeza mchanganyiko wa sodium hydroxide kwenye mawese,huku ukikoroga haraka haraka bila kusitisha ukitumia ubao .hii ni njia nzuri zaidi. Njia ya pili Chemsha mafuta kwenye joto la kadiri ya 55C Changanya maji na sodium hydroxide na uache mchanganyiko huu upoe hadi kufikia joto hilohilo. Baada ya kuandaa mchanyiko wako changanya vimiminika hivyo viwili huku ukikoroga kwanguvu sana kadiri uwezavyo, taratibu sabuni itageuka kuwa laini. Kabla...

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara, amewataka wanachi wilayani Tarime, kuachana na uwindaji haramu, badala yake watumie fursa zilizopo kukuza vipato vyao iii kuondokana na umasikini katika ngazi ya familia.  Pia, amewataka wananchi hao watumie fursa hizo kuwekeza katika miradi na biashara mbalimbali katika maeneo jirani na Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti, itakayowawezesha kuwaingizia vipato.  Waitara alitoa wito huo mjini Tarime, juzi, alipokutana na baadhi ya wananchi na kubadilishana nao mawazo, wakati akielekea nyumbani kwake k ij iji cha  Itiry o   kusherekea sikukuu ya Pasaka.  Alitoa ushauri kwa watu wenye nia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali wilayani humo, watumie nafasi hiyo iii kukuza na kuendeleza mji waTarime na wilaya hiyo kwa ...

Bei ya unga sasa ni mara 12 ya mfuko wa Simenti

Bei ya unga sasa ni mara 12 ya mfuko wa Simenti WAKATI bei ya unga wa sembe ikipanda mpaka kufikia kuuzwa kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500 kwa kilo, ile ya mfuko wa saruji wenye uzito wa kilo 50 imeshuka hadi sh. 9,000, sawa na Sh. 180 kwa kilo. Katika masoko na maduka mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambayo Nipashe ilitembelea jana, bei ya sembe ilikuwa ikiuzwa kwa kiasi hicho kwa rejareja huku wauzaji wa jumla wakiuza kiroba cha kilo 50 kwa kati ya sh.100,000 na sh.98,000. Ibrahim Omary, mfanyabiashara wa Kariakoo alisema anauza unga wa sembe kwa Sh. 2,400 kwa kuwa hununua kwa bei kubwa kutoka kwa wazalishaji. Alisema kampuni inayojulikana kwa jina la Mkulima huwauzia unga huo kwa Sh. 98,000 na Mama Neema huwauzia kwa sh. 100,000 kwa kiroba cha kilo 50. Kwenye baadhi ya maduka ya kula ya Kinondoni, unga umekuwa ukiuzwa kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500. Tandika bei ya wastani ni Sh. 2,200, Mwenge Sh. 2,400, Kimara sh. 2,500 na Yombo Vituka sh. 2,200. ...