Bunge lapinga ongezeko la ushuru vinywaji baridi
Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017 wenye marekebisho ya sheria 15 ikiwamo Sheria ya Ushuru wa Bidhaa.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji baridi umeongezeka kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61 ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi tatu.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepinga ongezeko hilo la shilingi tatu kwenye vinywaji baridi ikisema hatua hiyo itazorotesha ukuaji wa viwanda nchini.
Akiwasilisha Muswada huo jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema sheria hizo zinahusu masuala ya fedha, kodi, ushuru, tozo, na mawasiliano ili kupunguza, kurekebisha, au kufuta viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo mbalimbali ili kuboresha ukusanyaji wa kodi.
Dk Mpango alisema marekebisho hayo yamezingatia mkakati wa taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, na kwamba kiwango cha ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kimepunguzwa au kubakia ilivyo sasa.
Mengine aliyozungumzia ni ongezeko la ushuru katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa Sh 40, Sheria ya Benki Kuu inayorekebishwa ili kuweka sharti la ulazima kwa taasisi za serikali kufungua akaunti na kuhifadhi mapato na fedha Benki Kuu.
Alisema katika marekebisho hayo, pia ipo Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki ili kutoa wigo mpana kupanua wigo wa mauzo ya hisa za asilimia 25 zitakazouzwa na kampuni ya mawasiliano kwenye soko la hisa kwa kutoa fursa kwa Watanzania walio ndani na nje ya nchi, taasisi ya Kitanzania, kampuni zinazomilikiwa kwa pamoja baina ya Watanzania na raia wa nje, raia, kampuni na taasisi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au raia na kampuni kutoka nchi nyingine.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Hawa Ghasia alipinga kuongezeka ushuru kwa vinywaji baridi akisema hatua hiyo itapunguza uzalishaji.
Alitolea mfano hatua ya serikali ya kutoongeza kodi kwenye bidhaa hiyo kwa miaka mitatu iliyopita kuwa uzalishaji na uchumi uliongezeka na serikali kupata kodi; huku akipendekeza tozo 14 zilizobakia katika shule na vyuo binafsi zizidi kuondolewa ili wapunguzia gharama.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), alisema muswada huo umejumuisha asilimia 80 ya mapendekezo ya wabunge na kutaka asilimia 15 ya fedha ambazo mashirikia ya umma hutakiwa kuchangia mfuko mkuu wa serikali, zisitozwe kodi kwani mashirika ya umma yanalipa kodi mara mbili.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alipendekeza kuongezwa tozo ya asilimia sita hadi 12 kwenye mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha, na asilimia nane hadi 20 kwenye zawadi na pia kuongeza tozo ya leseni.