Skip to main content

Hatua 5 za kutatua tatizo lolote unalokutana nalo

Hatua 5 za kutatua tatizo lolote unalokutana nalo

Hatua ya kwanza; jua kwa undani tatizo ni nini. 
Najua utashangaa lakini ukweli ni kwamba wengi ambao wanakuwa na matatizo huwa hawajui tatizo hasa walilonalo ni nini. Na hivyo wanapokazana kulitatua wanashindwa, kwa sababu kama hujajua kiini cha tatizo huwezi kulitatua.

Mara nyingi watu wamekuwa wakiangalia madhara ya tatizo, badala ya kuangalia chanzo kikuu cha tatizo. Huwezi kutibu tatizo kwa kutibu madhara, badala yake unahitaji kuzama ndani na kujua chanzo hasa cha tatizo ni nini.

Na njia ya uhakika ya kufikia hilo ni kuuliza swali moja muhimu sana, KWA NINI. Uliza swali hili mara tano, yaani uliza kwa hatua tano. Kwa mfano kama tatizo lako ni kipato kidogo kwenye biashara yako, jiulize kwa nini kipato ni kidogo, jibu linaweza kuwa wateja ni wachache, jiulize tena kwa nini wateja ni wachache, hapo utapata majibu mengine, kwa kila jibu jiulize tena kwa nini? Mpaka utafika mahali na kuona hiki ndio kiini kikuu cha tatizo.

Lijue tatizo vizuri, wahenga walisema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. 

Hatua ya pili; orodhesha hatua unazoweza kuchukua. 
Baada ya kujua nini hasa ndiyo tatizo, sasa anza kuorodhesha kila hatua unayoweza kuchukua. Andika kila suluhisho linalowezekana kwenye tatizo ulilonalo.

Usijihukumu kwamba hiki kinawezekana au hakiwezekani, hiyo siyo hatua hii. Wewe hapa funguka na andika kila aina ya suluhisho unaloweza kufanyia kazi.

Hakikisha unakuwa muwazi na unaandika kila wazo linalokuja kwenye kichwa chako, hata kama litaonekana ni la hovyo au haliwezekani, wewe orodhesha. Ni kwa njia hii ndiyo unaweza kupata njia bora kabisa za kukabiliana na tatizo unalokutana nalo.

Hatua ya tatu; andika faida na hasara za kila suluhisho. 
Baada ya kuorodhesha hatua zote unazoweza kuchukua, yaani kila aina ya suluhisho unaloweza kuchukua, sasa unakwenda kuchambua suluhisho moja baada ya jingine.

Andika kila suluhisho na gawa pande mbili, upande mmoja andika faida utakayopata kama utachukua hatua hiyo, na upande wa pili andika hasara za kuchukua hatua hiyo.

Andika kila kitu ambacho unafikiria kuhusu suluhisho husika. Na fanya hivi kwa masuluhisho yote uliyoorodhesha kwenye hatua ya pili hapo juu.

Hatua ya nne; chagua suluhisho sahihi. 
Baada ya kujua faida na hasara za kila suluhisho, sasa unaweza kuchagua suluhisho sahihi kwako kufanyia kazi. Hapa angalia lile ambalo lina faida kubwa na nzuri na hasara kidogo.

Na unapoangalia mambo hayo kuwa makini usifumbwe macho na faida za muda mfupi ambazo mara nyingi zinakuja na hasara za muda mrefu.

Chagua suluhisho ambalo una uhakika unaweza kulifanya na hutokuja kujutia hapo baadaye. Pia hakikisha unaweza kusimamia suluhisho hilo bila ya kutetereka na kuweza kulitetea kwa wengine.

Hatua ya tano; fanya mapitio ya suluhisho ulilochukua. 
Ukishachukua hatua siyo mwisho, bali unahitaji kuwa unafanya mapitio na tathmini ya ile hatua uliyochagua kuchukua. Je inaleta matokeo ambayo ulitarajia kupata? Je kuna changamoto nyingine zinaibuka?

Bila ya kufanya tathmini unaweza kushangaa muda unakwenda lakini tatizo linaendelea kuwepo licha ya kupata suluhisho. Unapofanya tathmini unaona ni wapi panahitaji mkazo zaidi na wapi pako vizuri.

Hizo ndizo hatua tano muhimu za kufuata pale unapotaka kutatua tatizo lolote unalokutana nalo. Fuata hatua zote tano kwa mfuatano, usikimbilie hatua ya juu kama ya chini bado hujaikamilisha. Usiwe na haraka, ukishaingia kwenye matatizo unahitaji kutuliza akili yako ndiyo uweze kutatua matatizo hayo.

Kitu kingine muhimu sana kuzingatia ni uvumilivu, usitake kuchukua njia za mkato za kutatua tatizo lolote, maana njia hizi huwa zinaleta matatizo mengine makubwa zaidi.

Fanyia kazi njia hizi tano na kama kuna changamoto zaidi tuwasiliane kwa kutuandikia ujumbe wako kwenye page zetu za mitandao ya kijamii.

Popular posts from this blog

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara, amewataka wanachi wilayani Tarime, kuachana na uwindaji haramu, badala yake watumie fursa zilizopo kukuza vipato vyao iii kuondokana na umasikini katika ngazi ya familia.  Pia, amewataka wananchi hao watumie fursa hizo kuwekeza katika miradi na biashara mbalimbali katika maeneo jirani na Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti, itakayowawezesha kuwaingizia vipato.  Waitara alitoa wito huo mjini Tarime, juzi, alipokutana na baadhi ya wananchi na kubadilishana nao mawazo, wakati akielekea nyumbani kwake k ij iji cha  Itiry o   kusherekea sikukuu ya Pasaka.  Alitoa ushauri kwa watu wenye nia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali wilayani humo, watumie nafasi hiyo iii kukuza na kuendeleza mji waTarime na wilaya hiyo kwa ...

Ratiba ya Mkutano wa Saba wa Bunge Linaloanza Leo Jumanne April 4

Ratiba ya Mkutano wa Saba wa Bunge Linaloanza Leo Jumanne April 4 Waziri wa Fedha na Uchumi Dkt Philip Mpango anatarajiwa kusoma Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 siku ya Alhamisi, Juni 15 mwaka huu. Tarehe hiyo ni kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa Saba wa Bunge unaoanza leo  Jumanne (Aprili 4) katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, mkutano ambao ni maalum kwa ajili ya bajeti. Ratiba hiyo inaonesha shughuli ya kwanza kuwa ni uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki siku ya Jumanne, na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu itasomwa siku ya Alhamisi, Aprili 6 na kujadiliwa kwa siku nne, ikifuatiwa na bajeti ya Rais (siku 4) na Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Siku 1) kabla ya bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba Aprili 25. Mbali na bajeti za wizara, mkutano huo pia utajadili na kupitisha miswada kadhaa ya sheria ukiwemo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka, 2017 ==>Itazame hapa ratiba kamili ya mkutano huu...