Bei ya unga sasa ni mara 12 ya mfuko wa Simenti WAKATI bei ya unga wa sembe ikipanda mpaka kufikia kuuzwa kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500 kwa kilo, ile ya mfuko wa saruji wenye uzito wa kilo 50 imeshuka hadi sh. 9,000, sawa na Sh. 180 kwa kilo. Katika masoko na maduka mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambayo Nipashe ilitembelea jana, bei ya sembe ilikuwa ikiuzwa kwa kiasi hicho kwa rejareja huku wauzaji wa jumla wakiuza kiroba cha kilo 50 kwa kati ya sh.100,000 na sh.98,000. Ibrahim Omary, mfanyabiashara wa Kariakoo alisema anauza unga wa sembe kwa Sh. 2,400 kwa kuwa hununua kwa bei kubwa kutoka kwa wazalishaji. Alisema kampuni inayojulikana kwa jina la Mkulima huwauzia unga huo kwa Sh. 98,000 na Mama Neema huwauzia kwa sh. 100,000 kwa kiroba cha kilo 50. Kwenye baadhi ya maduka ya kula ya Kinondoni, unga umekuwa ukiuzwa kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500. Tandika bei ya wastani ni Sh. 2,200, Mwenge Sh. 2,400, Kimara sh. 2,500 na Yombo Vituka sh. 2,200. ...