Skip to main content

VIROBA Marufuku Kuanzia Leo

VIROBA Marufuku Kuanzia Leo

Mtakumbuka tarehe 20 Februari 2017 Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la Serikali la utaratibu utakaotumika kutekeleza agizo la kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba)kuanzia tarehe 1 Machi 2017. 

Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo, na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012.

Napenda kusisitiza na kuujulisha umma wa Tanzania kuwa utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali kuhusu usitishaji uingizaji, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki vya kufungia pombe kali utaanza rasmi tarehe 01 Machi, 2017, katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Operesheni ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe 2 Machi 2017 kwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa. 

Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mnamo terehe 24 Februari 2017, kiliitishwa kikao cha Mawaziri na viongozi wa taasisi za Serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hili. Katika kikao hicho, Wizara na taasisi za Serikali zilipewa majukumu mbalimbali, kama ifuatavyo:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki. Aidha, Mamlaka itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol) wamesajiliwa na kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa.

Wazalishaji na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale tu ambao wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu (3) ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa. Uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali ambao hawajasajiliwa itakuwa ni kosa la jinai kulingana na Sheria.

Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani, atasajili makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani nchini ikiwa ni pamoja na Ethanol. 

Msajili atawajibika kutoa taarifa sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi na taasisi zinazohusika, kiasi kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na madhumuni ya matumizi.

Kulingana na sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka 2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika operesheni hii itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama vimekidhi viwango vya kitaifa Ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali.

Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha bidhaa zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa ufafanuzi wa hatima ya mitambo hiyo. Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia vifungashio vya plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashtakiwa.

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mabwana afya katika operesheni hii watatoa elimu kwa umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza vileo vya aina zote, na kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume cha sheria na kanuni.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili. 
 
Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia.

Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni.

Kama tangazo letu la tarehe 20/2/2017 lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji muda mchache kufanya hivyo, na ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata kibali maalum kabla ya tarehe 28/2/2017. 

Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya wazalishaji 9. Tutangaza kesho iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au la. Kanuni za upigaji marufuku pombe hizi zipo tayari.

Pia tumepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hili limekuja ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala. Ukweli ni kwamba Serikali ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei 2016, na mara kadhaa baada ya hapo, na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi.

 Vilevile, taarifa ya Serikali iliyotangaza kupiga marufuku pombe za viroba ziliripotiwa kwa ukubwa stahiki kwenye vyombo vya habari, ikiwemo kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi, mwezi Agosti 2016. 

Katika taarifa zote za nyuma, Serikali ilitangaza kwamba hatua hiyo itaanza tarehe 1 Januari 2017. Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili. 

Iwapo, baada ya taarifa hizo za Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au kutengeneza au kuhifadhi pombe za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo, atakuwa amefanya hivyo akijua madhara yake.

Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.

OFISI YA MAKAMU WA RAIS
28/02/2017

Popular posts from this blog

Jinsi ya kutengeneza SABUNI ya kipande YA KUGANDISHA

Jinsi ya kutengeneza SABUNI ya kipande YA KUGANDISHA Utengenezaji wa sabuni hii una njia nyingi Hatua  ya kwanza Chemsha vipimo 7 vya mafuta ya mawese au mafuta ya shea hadi ifikie hatua ya kimiminika chuja na yaweke kwenye chungu cha mfinyanzi au chombo cha plastiki. Hatua ya pili Pima vipimo 5 vya maji baridi kwenye chombo cha plastiki ongeza kipimo 1cha sodium hydroxide kwa uangalifu mkubwa kwenye maji acha hadi mchanganyiko huo uyeyuke. Subiri mchanganyiko wa sodium hydroxide na mafuta ukaribie kupoa. Hatua ya tatu Taratibu ongeza mchanganyiko wa sodium hydroxide kwenye mawese,huku ukikoroga haraka haraka bila kusitisha ukitumia ubao .hii ni njia nzuri zaidi. Njia ya pili Chemsha mafuta kwenye joto la kadiri ya 55C Changanya maji na sodium hydroxide na uache mchanganyiko huu upoe hadi kufikia joto hilohilo. Baada ya kuandaa mchanyiko wako changanya vimiminika hivyo viwili huku ukikoroga kwanguvu sana kadiri uwezavyo, taratibu sabuni itageuka kuwa laini. Kabla...

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime

Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara akemea uwindaji haramu Tarime MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Jenerali George Waitara, amewataka wanachi wilayani Tarime, kuachana na uwindaji haramu, badala yake watumie fursa zilizopo kukuza vipato vyao iii kuondokana na umasikini katika ngazi ya familia.  Pia, amewataka wananchi hao watumie fursa hizo kuwekeza katika miradi na biashara mbalimbali katika maeneo jirani na Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti, itakayowawezesha kuwaingizia vipato.  Waitara alitoa wito huo mjini Tarime, juzi, alipokutana na baadhi ya wananchi na kubadilishana nao mawazo, wakati akielekea nyumbani kwake k ij iji cha  Itiry o   kusherekea sikukuu ya Pasaka.  Alitoa ushauri kwa watu wenye nia ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali wilayani humo, watumie nafasi hiyo iii kukuza na kuendeleza mji waTarime na wilaya hiyo kwa ...

SADC YALIPONGEZA BARAZA LA USALAMA LA UN KWA KUONGEZA MUDA KWA MISHENI YA ULINZI DRC

SADC YALIPONGEZA BARAZA LA USALAMA LA UN KWA KUONGEZA MUDA KWA MISHENI YA ULINZI DRC 1 2 3 4 5 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York, Marekani na kupitisha Azimio la kuongeza muda kwa vikosi vya usalama vilivyopo DRC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy. Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Mahiga (hayupo pichani). Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb). akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani. TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa...